URAISI 2015: KUA NA MIDAHARO YA WAGOMBEA URAISI ~ :: Habari Duniani

Dar es Salaam. Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) na ITV/ Radio One wamesaini makubaliano ya kuandaa midahalo ya wagombea wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Udasa, Profesa Kitila Mkumbo alisema katika nchi za kidemokrasia midahalo hufanikisha uchaguzi ulio huru, haki na wazi.
Pia, alisema midahalo hiyo hutoa fursa muhimu kwa wagombea kueleza falsafa, sera na mikakati yao ya kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi.
Hata hivyo, Profesa Mkumbo alisema midahalo watakayoendesha haitaegemea chama chochote na kwamba mgombea atakayekataa kushiriki hawamlazimishi.
“Hatutakuwa na uwezo wa kumlazimisha mgombea, nchi hii ina historia ya wagombea kukimbia midahalo,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema muda rasmi wa kuanza kwa midahalo hiyo utatangazwa baadaye, wananchi wajue kuwa kupitia matangazo hayo wapiga kura watajua weledi na umahiri wa wagombea na vyama vyao.
“Tafiti zinaonyesha kuwa midahalo ya wagombea urais ina nafasi ya kipekee katika kuwawezesha wapiga kura kuamua mgombea gani wamchague,” alisema.
Alisema kuwa vyama vyote vitakavyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na ambavyo vitasimamisha wagombea wa urais vitaalikwa kushiriki katika midahalo hiyo.
Pia wagombea wote watakaojitokeza kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu wataalikwa kushiriki mdahalo huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile alisema midahalo hiyo itaaminiwa na wananchi kwa sababu wanaoandaa hawagombei nafasi yoyote katika uchaguzi huo.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

SOCIALIZE

IN CASE YOU MISSED IT

FOR INSURANCE SERVICES CLICK HERE